WIZARA ya Maliasili na Utalii imekamata makontena 31 ya magogo aina ya mitiki na misandali yenye thamani ya Sh milioni 300 yaliyokuwa yanasafirishwa kinyume cha sheria kwenda Mashariki ya Mbali.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana katika eneo Nasaco yalikohifadhiwa makontena hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru alisema watuhumiwa walidai kuwa magogo hayo yalitoka Zambia na nyaraka husika zipo Tunduma.
"Tumebaini kuwa upo mtandao wa kihalifu unaovuna rasilimali zetu za misitu kuandaa nyaraka bandia za kusafirisha magogo nje ya nchi. Hata kama nyaraka hizo zingekuwepo ni batili maana Tanzania hairuhusu uuzaji wa magogo nje ya nchi. Wahusika wote watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria," alisema.
Aliongoza kuwa tayari ofisi yake imeshawasiliana na TRA Tunduma kujiridhisha juu ya uhalali wa nyaraka hizo (kama kweli zipo) ili kuufumua mtandao wote wa wizi na kufuatiwa na hatua zaidi za kisheria.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa magogo yanavunwa kinyume cha sheria sehemu mbalimbali za nchi kama Mbeya, Songea na kwingineko na wahusika kuandaa nyaraka za uongo kuonesha kuwa magogo hayo yanatoka nje ya nchi.
"Leo hapa tunaye Balozi Mdogo wa Zambia, Elizabeth Phiri ambaye amethibitisha pasi na shaka kuwa magogo hayo hayajatoka nchini Zambia kama yeye mwenyewe alivyofafanua wakati wa ukaguzi jijini Dar Salaam," alisema.
Balozi Phiri alisema Zambia imepiga marufuku uuzaji wa magogo nje ya nchi hivyo nyaraka zinazodaiwa kuonesha kuwa magogo hayo yanatoka Zambia hazitakuwa na uhalali wowote.
"Zambia hatuuzi magogo nje ya nchi bali tunauza mazao ya mbao. Tusubiri tuone nyaraka zinazodaiwa kutoka Tunduma tuweze kupima ukweli wenyewe," Balozi Phiri alisema.
"Zambia hatuuzi magogo nje ya nchi bali tunauza mazao ya mbao. Tusubiri tuone nyaraka zinazodaiwa kutoka Tunduma tuweze kupima ukweli wenyewe," Balozi Phiri alisema.


Post a Comment