Utathmini wa takwimu kuhusu watoto wanaozaliwa Uingereza umebaini mimba
nyingi hutungwa wakati wa Krismasi kuliko wakati mwingine wowote ule wa
mwaka.
Takwimu hizo za kipindi cha miongo miwili kutoka Idara ya Taifa ya
Takwimu zinaongeza watoto wanaozaliwa huongezeka sana wiki 40 (miezi 9)
baada ya msimu wa sikukuu.
Hili huenda linatokana na wanandoa kutumia muda mwingi pamoja
wakisherehekea, au kulenga makusudi mwanzo wa mwaka mpya wa shule ambao
huanza mapema Septemba nchini humo.
“Ongezeko la watoto wanaozaliwa mwishoni mwa Septemba ni ishara kwamba
mimba nyingi hutungwa wiki chache kabla ya Krismasi na kuendelea hadi
siku chache baada Krismasi kuliko wakati mwingine wowote wa mwaka,”
idara hiyo imesema.
Kawaida watoto 1,800 huzaliwa kila siku lakini idadi hii hupanda hadi
1,974 siku yenye kuzaliwa watoto wengi zaidi ambayo ni Septemba 26.
Siku zinazoshuhudia idadi ndogo zaidi ya watoto wanaozaliwa ni siku za Krismasi, Boxing Dei na siku ya Mwaka Mpya.
Hili sana huenda linatokana na idadi ndogo ya watu wanaopangiwa
kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji siku hizo, kwani huwa ni siku za
mapumziko.
Profesa wa masuala ya uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield Allan Pacey
ameambia BBC: “Wazo kwamba mimba nyingi hutungwa wakati wa Krismasi lina
msingi. Nina uhakika sherehe na shamra shamra za wakati huu huchangia.”


Post a Comment