CUF yamwandikia waraka Mwenyekiti wa ZEC

Baadhi ya viongozi wa CUF, Nassor Mazrui, Mansour Yusuf Himid, Imsail Jussa Ladhu wakizungumza na wanahabari.
Baadhi ya viongozi wa CUF Bw. Nassor Mazrui, Mhe. Mansour Yusuf Himid na Ismail Jussa, wakizungumza na waandishi wa habair mapema hii leo
Chama Cha Wananchi (CUF) kimemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha juu ya ucheleweshaji wa utangazaji wa matokeo ya uchaguzi ambapo inaingia siku ya tatu sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho Mtendeni Mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema lengo la barua hiyo ni kutaka kujua lini na saa ngapi tume hiyo itatangaza matokeo yote pamoja na kumtangaza mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar.
“Tunataka kujua ni lini na saa ngapi mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar atatangazwa,” alisema Mazrui.
Kwa mujibu wa kifungu cha 42 (4) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanapaswa kutangazwa ndani ya kipindi cha siku tatu tokea siku ya kupiga kura.
“Tumemwambia Mwenyekiti wa tume kwenye barua yetu kwamba ni vyema sasa tukajua siku na wakati wa kutangaza matokeo hayo ili tujitayarishe na hatua zinazofuata, tumemwambia tunapenda pia kujua utaratibu wa kumuapisha Rais mpya mara baada ya matokeo kutangazwa,” alisema Mazrui.
Hata hivyo CUF imemtaka Mwenyekiti awapatie majibu yanayoridhisha katika hatua hizo zilizobaki za uchaguzi mkuu huku wakitambua macho na masikio yote ya walimwengu yakiwaangalia na kusikiliza uchaguzi huu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.
“Ulimwengu wote unatusikiliza sisi jinsi tutakavyokamilisha uchaguzi huu na kuheshimu maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura.” Alisema.
Katika hatua nyengine chama hicho kimetoa wito kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho na Wazanzibari wote kwa ujumla kuendelea kubaki watulivu na kutunza amani ya nchi, wakati CUF ikijiandaa kufanya kazi na kila Mzanzibari bila ya kujali itikadi yake kwa lengo la ujenzi wa Zanzibar mpya.
Aidha chama hicho kimesema kimepata taarifa kwamba juzi usiku majira ya saa tatu usiku Mweyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar alisema anaumwa na hivyo kudai hawezi kusaini fomu za matokeo yaliokwisha kuhakikiwa na maafisa wa tume na mawakala wa wagombea urais.
“Baada ya hapo Mwenyekiti akasita kuendelea na kazi ya kutangaza matokeo. Hadi jana (juzi) usiku ni matokeo ya majimbo 13 tu yaliokwisha kutangazwa,” alisema Mazrui.
Alisema wameona kuna mkakati wa makusudi kwamba matokeo yote yaliotangazwa hadi sasa ni yale yanayotoka katika majimbo ambayo CCM iliongoza.
“Kati ya majimbo 13 yaliotangazwa matokeo jana, ni jimbo la Malindi tu ambalo CUF iliongoza ndilo ililiotangazwa, inashtaajabisha kuwa hadi sasa tume haijatangaza matokeo hata jimbo moja la Pemba” aliongeza Mazrui.
Alisema matokeo ya majimbo mengine maneno ya Unguja ambayo pamoja na lile la Malindi CUF imeongoza ambapo alisema jambo hilo haliashirii nia njema na wanaamini lina lengo la kuwafanya watu waamini kwamba CCM inaongoza uchaguzi huo jambo ambalo sio la kweli.
“Pengine kuna lengo la kuja kuyachakachua matokeo ya majimbo ambayo CUF iliongoza ili kulazimisha ushindi wa CCM ambao haupo,” alisema.
CUF wanasema ucheleweshaji huo unaofanywa na tume ya uchaguzi hauna sababu yoyote na una lengo la kuwatia khofu wananchi wa Zanzibar na kuiweka nchi katika wasiwasi pasipo na sababu.
“Kama tunavyojua, kutokana na utaratibu uliowekwa na tume wa kupatikana kila chama kilichoweka mgombea, kupitia mawakala wetu nakala ya matokeo ya kila kituturi cha kupigia kura na nakala ya fomu ya majumuisho kwa kila jimbo sisi CUF tunayo,” alisema Mazrui.
CUF ilisema haino sababu ya ucheleweshaji wa matokeo hasa kwa kuzingatia kura zilishahesabiwa na fomu za vituoni na za majumuisho kwa majimbo yote ya Unguja na Pemba kupatikana ambapo kila chama kimepewa nakala zake.
“Wananchi wa Zanzibar wamefanya maamuzi yao kwenye visanduku vya kura na sasa wana hamu ya kujua matokeo ya kazi yao nzuri,” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.[via Salma Said | ZanzibariYetu](P.T)

0/Post a Comment/Comments

Stay Conneted

{ads}